emblem

Energy and Water Utilities Regulatory Authority Consumer Consultative Council

EWURA CCC

News

Watoa huduma waaswa kuzingatia haki za walemavu


Wito umetolewa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga UWSA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu wa kusikia kila wanapotoa taarifa kuhusu huduma za maji na umeme.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania mkoa wa Tanga (CHAVITA) bi Selina Mlemba wakati wa semina ya uelimishaji kwa kundi la watu wenye ulemavu, iliyofanyinka hivi karibu jijini Tanga, na kuwakutanisha washiriki kutoka makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu jijini humo.

Bi Mlemba alisema kuwa, walemavu wa kusikia wamekuwa wahanga wakubwa wa kukosa taarifa kuhusu huduma za nishati na maji kwa kuwa njia za mawasiliano zinazotumiwa na watoa huduma kutoa taarifa mbalimbali hazizingatii kundi la watu wenye mahitaji maalum kama viziwi.

“Mmetufundisha kuwa kuna haki ya kupata taarifa, lakini tujiulize taarifa mbalimbali kama vile za katizo la huduma na zinginezo watoa huduma wanazitoaje? Je kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia nalo limefikiriwa kuwa lina haki ya kupata taarifa hizo kama yalivyo makundi mengine?,” alihoji bi Mlemba na kuongeza kuwa, wakati sasa umefika watoa huduma wabadilike kwa kuwa huduma wanazotoa si za kibaguzi bali zinatumiwa na watu aina zote.

Bi Mlemba alisema, imekuwa desturi kwa watoa huduma wengi kupita mitaani na vipaza sauti wakitangaza taarifa mbalimbali kuhusu kulipa madeni, katizo la huduma na zingine kama hizo ama kutumia redio kutoa matangazo bila kujali kuwa katika jamii pia kuna walemavu wa kusika ambao yamkini wanahitaji njia mbadala ya kupata taarifa.

Akijibu hoja hiyo, Ofisa Mkuu Huduma kwa Wateja kutoka TANESCO mkoa wa Tanga bi Monica Mabada, alikiri kuwepo kwa changamoto kwenye upande wa mawasiliano kati ya taasisi yake na kundi la walemavu wa kusikia na kuahidi kuwa, changamoto hiyo ataifikisha kwenye ngazi ya juu ya uongozi ili ifanyiwe kazi.

“TANESCO tunazo njia nyingi za mawasiliano tunazotumia kuwasiliana na wadau wetu ikiwemo utoaji wa taarifa. Ninakiri huenda hatufanyi ipasavyo kwa upande wa kufikisha taarifa kwa kundi la walemavu wa kusikia, lakini hili tumelichukua na tutalifanyia kazi ili kuboresha utoaji wa taarifa kwa makundi yote,” alieleza bi Mabada.

Aidha, aliwaomba watu wenye ulemavu ambao wana simu janja na walioko tayari kuorodhesha namba zao kwenye karatasi maalumu aliyoitoa wakati wa mafunzo hayo ili waweze kuingizwa kwenye kundi la wateja wa TANESCO wanaotumia mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambako Shirika hilo huwasiliana na wateja wao moja kwa moja kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno.

“Ninawaomba muorodheshe majina yenu, tutawaingiza huko ili iwe rahisi kwa kundi lenu pia kupata taarifa na hata nyie kutoa taarifa,” alisisitiza.

Awali akifungua semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumiaji mkoa wa Tanga ndugu Andrew Nkuzi aliwaomba washiriki wa semina hiyo, wawe wasikivu wakati wote wa mafunzo na kuuliza maswali ama kuomba ufafanuzi wa jambo lolote bila woga.

Alisema, kundi la watu wenye mahitaji maalumu ni kundi muhimu kwa kuwa mara nyingi limekuwa ni kundi linalosahaulika katika masuala ya kujifunza.

Aliwaasa washiriki wa kundi hili kuwa mabalozi wazuri kwenye jamii zao kwa kuwashirikisha watu wengine kwenye jamii yao kuhusu vitu watakavyojifunza ili waweze kuchangia vema katika kuboresha huduma za nishati na maji nchini.

Kundi la watu wenye ulemavu ni moja ya makundi muhimu ambayo EWURA CCC imepanga kuendelea kutoa elimu kwao ili kuwajengea uwezo na uelewa wa kuzifahamu haki zao na kuzidai ili kutoa mchango katika kuboresha huduma za nishati na maji nchini.