News
Wahofia usalama wao kutoa taarifa wizi wa maji
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameeleza sababu inayowafanya wasitoe taarifa za wizi wa maji na uhujumu wa miundombinu ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) wakidai kuwa ni hofu waliyonayo kuhusu usalama wao.
Akiongea wakati wa maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DIFT) 2019, mkazi wa Ubungo, ndugu Francis Kambaya alieleza kuwa, wananchi wengi hawatoi taarifa kuhusu wizi wa maji na uhujumu miundombinu kwa kuwa wanahofia usalama wao na mali zao baada ya kutoa taarifa husika.
“DAWASA inaibiwa maji mengi na ukweli ni kuwa, jamii inawafahamu wezi hao wa maji. Tatizo ni kuwa hakuna uhakika wa usiri wa taarifa unazotoa. Mwisho wa siku unaweza kuishia kuingia kwenye uhasama na wanaojihusisha na wizi huo na ukafanyiwa jambo baya,” alisema ndugu Kambaya.
Aliishauri DAWASA kuunda vikosi vya ukaguzi kwenye kanda mbalimbali ili visaidie kubaini wezi hao kwa lengo la kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
“DAWASA inapaswa kuunda vikosi vya watu wachache wachache na wapewe huduma ya pango kwenye maeneo ambayo wizi wa maji umekithiri, ili watu hao watakaokuwa kwenye vikosi hivyo, wajichanganye na wakazi wa maeneo hayo ilhali wakijua kuwa wako kwenye kazi maalumu ya kubaini wezi wa maji na hatimaye kutoa taarifa zenye uhakika zitazowezesha kukamatwa kwa wanaojihusisha na wizi huo,” alisisitiza ndugu Kambaya.
Aidha, aliishauri DAWASA kushusha bei ya maji kwa kuwa bei ya sasa ya TZS 1,663 kwa wateja wa majumbani ni kubwa na kudai kuwa huenda ikawa inachagiza wimbi la wizi wa maji hususan kwa familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama hizo.
Ndugu Kambaya aliushauri uongozi wa DAWASA pia kuona umuhimu wa kuwafundisha na kuwakumbusha kila wakati watumishi wake kuhusu maadili ya utumishi kwa kuwa, baadhi yao wanatuhumiwa kujihusisha na vishoka.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) Mhandisi Goodluck Mmari kwa nyakati tofauti amekuwa akiwasihi wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake kutokuwa na woga wa kutoa taarifa za wizi ama uhujumu miundombinu, kwa kuwa kutofanya hivyo kunaongeza bei ya huduma ya maji jambo ambalo halina tija kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Mkumbuke tu kwamba, bei za maji zinazotozwa sasa zinajumuisha maji yote yanayozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wateja wa DAWASA na mamlaka zingine, na kuwa gharama za maji yanayopotea zimeunganishwa kwenye gharama wanazotozwa wateja wote. Je, lipi jambo jema, kufumbia macho wizi na upotevu huo wa maji ili wananchi wasio na hatia waendelee kuwalipia wanaoiba maji? au kutoa taarifa ili wezi hao washughulikiwe?,” alihoji Mhandisi Mmari.
Katika programu zake za uelimishaji, EWURA CCC imekuwa ikielimisha watumiaji wa huduma za nishati na maji kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo haki na wajibu wa mtumiaji, matumizi sahihi ya huduma, kanuni za ubora wa huduma na utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wananchi kufanya maamuzi sahihi kila wakati.
EWURA CCC imejipanga vema kutekeleza jukumu lake la kutoa elimu kwa umma, kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya wadau kupitia njia tofauti za mawasiliano kama zilivyoainishwa kwenye mkakati wake wa mawasiliano.