emblem

Energy and Water Utilities Regulatory Authority Consumer Consultative Council

EWURA CCC

News

RC Senyamule- “Baada ya Nanenane, Tukutane Vijijini”


RC Senyamule- “Baada ya Nanenane, Tukutane Vijijini”

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, amepongeza jitihada za Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) katika kuelimisha wananchi kuhusu matumizi salama na endelevu ya huduma za nishati na maji, huku akisisitiza kuwa elimu hiyo isibaki kwenye maonesho pekee bali ifikishwe hadi vijijini.

Akizungumza Agosti 5, 2025 baada ya kutembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Kilimo (Nanenane), Mhe. Senyamule alisema:

“Nawapongeza sana EWURA CCC kwa kazi kubwa mnayofanya. Elimu mnayotoa kuhusu matumizi salama na endelevu ya huduma za maji, na nishati ni ya msingi sana kwa maendeleo ya taifa letu. Lakini kazi yenu isiishie Nanenane tu. Baada ya maonesho haya, tukutane vijijini.”

Mhe. Senyamule alisisitiza umuhimu wa wananchi kuelimishwa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya ya familia na mazingira.

Kwa upande wake, Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Bw. Lugiko L. Lugiko, alieleza kuwa Baraza linaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA kwa kuhimiza matumizi salama na endelevu ya nishati na maji.

“Miongoni mwa mikakati yetu ni kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu ya maji na umeme, kutumia nishati safi ya kupikia, na kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa pindi wanapopata changamoto kwenye huduma wanazopokea,” alisema Bw. Lugiko.

Akiitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Bw. Lugiko alibainisha kuwa EWURA CCC tayari imeandaa mpango wa kufikisha elimu hiyo vijijini kupitia redio, mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya mawasiliano.

“Tumejipanga kuwafuata wananchi popote walipo kwa kutumia teknolojia kwa sababu maslahi yao ndiyo msingi wa uwepo wetu kama Baraza,” alisisitiza.

Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa EWURA CCC kuwasiliana moja kwa moja na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuwapa elimu ya msingi kuhusu haki, wajibu na usalama wa huduma za nishati na maji.