emblem

Energy and Water Utilities Regulatory Authority Consumer Consultative Council

EWURA CCC

News

EWURA CCC yaadhimisha wiki ya mtumiaji


Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) kwa kushirikiana na taasisi zingine za kumtetea mtumiaji chini ya mwavuli wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania, limeshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Mtumiaji Duniani ambayo kilele chake huadhimishwa tarehe 15 Machi kila mwaka.

Maadhimisho hayo ambayo yaliongozwa na kaulimbiu ya “Fursa, Haki na Wajibu wa Mtumiaji Kuelekea Uchumi wa Viwanda” yalilenga kufanya majadiliano na washiriki kutoka makundi mbalimbali ili walijue Baraza na majukumu yake na kuzitambua fursa zilizopo kwenye huduma za nishati na maji zinavyoweza kuchangia katika kuufikia uchumi wa viwanda.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye chuo cha Uhasibu Arusha kwa njia ya mikutano na kuwakutanisha wadau 1,038 kutoka makundi mbalimbali ya watumiaji jijini Arusha, wakiwemo viongozi wa AZAKI na Serikali za Mitaa, wanafunzi wa shule za sekondari na washiriki kutoka vyuo.

Katika wasilisho lake kwa makundi yote manne ya wadau, EWURA CCC ilizitaja fursa zilizopo kuwa ni pamoja na uunganishwaji wa nishati ya umeme kwa gharama ndogo ya TZS 27,000 kwa wakazi wa vijijini, nafasi za masomo katika taaluma za mafuta na gesi na uwekezaji wa Serikali kwenye miradi mikubwa ya umeme na maji, miradi ambayo inaongeza fursa na uhakika wa upatikanaji wa huduma za nishati na maji, ambazo ni chachu katika kuufikia uchumi wa viwanda.

Wakichangia mada kwenye wasilisho la EWURA CCC wakati wa maadhimisho hayo, pamoja na kuwashukuru waandaaji, wadau hao walishauri umuhimu wa Mamlaka za Maji mijini kushirikisha wadau wake pindi wanapoona uhitaji wa kuomba ongezeko la bei ya huduma badala ya mfumo unaotumiwa sasa wadau wengi kualikwa tu kwenye mikutano ya taftishi ambapo ni nadra maoni yao kufanyiwa kazi.

“Tunapoongelea fursa kuelekea uchumi wa viwanda, ni vema tukaangalia pia na namna bei za huduma muhimu kama maji zinavyochangia ama kukwamisha kuufikia uchumi wa viwanda. Ushirikishwaji wa wadau katika zoezi hili la upangaji wa bei ni la muhimu na tunaomba maoni yao yawe yanazingatiwa, ” alieleza mmoja wa washiriki.

Alisema kuwa, kama gharama za huduma kama maji na umeme zitakuwa ni za kawaida ni wazi kuwa watu wengi wataunganishwa na huduma hizo na hiyo itakuwa ni fursa kwao kutumia muda wao kushughulikia masula ya uzalishaji badala ya kuhangaika na utafutaji wa huduma hizo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya kupanga bei, Katibu Mtendaji wa Baraza Mhandisi Goodluck Mmari alisema kuwa, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira hutumia miongozo na kanuni za EWURA zinazoelekeza utaratibu mzima wa kuomba kupandisha, kurasimisha ama kushusha bei na si kweli kuwa Mamlaka hizo zina utashi wa kupandisha kila wakati zikijisikia kufanya hivyo.

Aidha, Mhandisi Mmari alieleza uk. 8 EWURA CCC yaadhimisha Siku ya Mtumiaji Katibu Mtendaji wa EWURA CCC Mhandisi Goodluck Mmari, akitoa ufafanuzi kuhusu utaratibu unaotumiwa na Mamlaka za Maji nchini kuomba kwa Mdhibiti idhini ya kupandisha bei ya huduma.

Aidha, Mhandisi Mmari alieleza kuwa mikutano ya wadau inalenga kumwezesha Mdhibiti ambaye ni EWURA kukusanya maoni kutoka kwa wadau, maoni ambayo huisaidia wakati wa uchambuzi wa maombi ya bei ya Mamlaka husika, ili kufikia maamuzi sahihi ya kiasi kinachopaswa kupanda ama kutokupandisha kabisa. ”Ndugu zangu, kwanza kabisa ninasisitiza kuwa suala la ushiriki kwenye mikutano ya taftishi ni la muhimu kweli kwetu sote, licha ya kuwa Baraza linatoa uwakilishi wenu katika mikutano kama hiyo kama Sheria inavyoelekeza.

Lakini pili, mnaposhiriki mikutano hiyo, maoni mnayotoa hapo siyo kwamba ndiyo maamuzi ya mwisho bali yanasaidia Mdhibiti wakati wa uchambuzi wa maombi husika ili kufikia maamuzi sahihi kuhusu bei inayotarajiwa kupitishwa. Mnaposhiriki kwa wingi na kutoa maoni mnachangia kwenye upatikanaji wa bei ambayo watu wengi wataimudu,” alifafanua Mhandisi Mmari. Nchini Tanzania, maadhimisho ya Siku ya Mtumiaji Duniani huratibiwa na taasisi wanachama wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) linaloundwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri ya Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC) Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA CCC) Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC), Tume ya Ushindani (FCC) na Baraza la Ushindani (FCT)