News
Baraza lafunda vijana 150 Lindi

Kamati ya watumiaji ya EWURA CCC mkoani Lindi, imeshiriki kwenye maonesho ya wiki ya vijana kitaifa na kuelimisha zaidi ya wadau 150 kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma za nishati na maji zinazodhibitiwa na EWURA.
Akiongea wakati wa maonesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mpilipili, Manispaa ya Lindi kuanzia tarehe 08 hadi 14 Oktoba 2019, Mwenyekiti wa Kamati ya watumiaji ya Mkoa wa Lindi Bibi Angelina Murangira, alitaja malengo ya ushiriki wa Baraza katika maonesho hayo kuwa ni pamoja na kuitangaza EWURA CCC, ili itambulike miongoni mwa wadau na waitumie kunapokuwa na uhitaji.
Alitaja malengo mengine kuwa ni pamoja na kukutana na wadau ambao siyo rahisi kuwafikia kwa kutumia njia zingine, kujibu maswali na kutatua changamoto zinazoibuliwa na wadau.
“Matukio kama haya ni muhimu sana kwa taasisi kama EWURA CCC kushiriki kwa kuwa tunawafikia wadau muhimu mno ambao tusingeweza kuwafikia kwa kutumia njia nyingine yoyote ile,” alisisitiza Bibi Murangira.
Alisema maonesho ya wiki ya vijana 2019, yamekuwa ni miongoni mwa maonesho ambayo yamepata mwitikio mkubwa wa wadau kutembelea banda la Baraza na kwa kupitia maonesho hayo, Baraza limepata fursa nzuri kuelimisha na kujibu hoja zilizojitokeza.
“Vijana wengi walihoji tatizo la uhaba wa maji kwenye maeneo mengi ya Manispaa ya Lindi. Bahati nzuri tuliwaelimisha mipango ya LUWASA ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wengi zaidi,” alieleza Bi. Murangira.
Alisema njia zilizotumiwa na Kamati yake katika kutoa elimu kwa makundi ya vijana ni pamoja na utoaji wa elimu kwa kila kundi kama darasa, na majadiliano.
Bi Murangira aliyataja maeneo ya uelimishaji yaliyotolewa wakati ya maonesho hayo kuwa ni pamoja na elimu kuhusu uwepowaEWURACCC namajukumu yake, haki na wajibu wa mtumiaji, matumizi sahihi ya huduma na namna ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko.
“Ilikuwa ni muhimu kuwaelimisha vijana na hata wadau wengine waliotembelea banda la EWURA CCC kuhusu haki na wajibu wao kwa kuwa, kufanya hivyo kunawaandaa kuwa na uwezo wa kudai haki hizo zinapokiukwa,” alieleza bi Murangira na kuongeza kuwa elimu kwa mtumiaji inakiweka kizazi cha sasa kwenye nafasi nzuri ya kuchangia katika kuboresha huduma za nishati na maji.
Nao baadhi ya wadau waliotembelea banda hilo walionesha wazi kuridhishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuelimisha ndugu na marafiki zao ili kuwa na makundi ya watumiaji yanayoweza kujisimamia na kupigania haki zao.
Kamati ya EWURA CCC mkoani Lindi imejipanga kuyafikia makundi mengine mengi katika jamii kwa kupitia mikusanyiko, makongamano na semina ili kuelimisha na kuhamasisha umuhimu wa ushiriki wao katika uboreshaji wa huduma za nishati na maji mkoani humo.
Na Jumbe Kawambwa